MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameilekeza Wizara ya Madini na Taasisi zake kuelekeza nguvu katika mikoa yenye madini mkakati ikiwemo Dodoma kufanyiwa utafiti wa kina wa haraka ili kufikia asilimia 50 kabla ya mwaka 2030. Dkt. Mpango ameyasema hayo leo Juni 20, 2024 katika ufunguzi wa Kongamano la Wachimbaji Madini wakati akitembelea mabanda ya maonesho yanayokwenda sambamba na mkutano wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) lililoanza leo hadi Juni 27 katika viwanja vya Jakaya Kikwete Conventional Centre (JKCC) mkoani Dodoma. Amesema kwamba mkakati wa Wizara kupitia vision 2030: yenye kauli mbiu ya madini ni maisha na utajiri itachukua muda mrefu na kwamba miaka sita kutoka sasa ni mingi na kuagiza utafiti huo ufanyike haraka. Kwa sasa utafiti wa kina uliofanyika kwa nchi nzima ni asilimia 16 na malengo ya vision 2030 ni kufikia angalau asilimia 50 ifikapo mwaka huo. Akizungumzia mazingira ya uwekezaji Dkt. Mpango amesema, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara ya Madini kwa wachimbaji wadogo ambapo sasa idadi ya vituo vya ununuzi wa madini imefikia 100 na masoko ya madini 42. Ameongeza kuwa, uchimbaji mdogo wa madini unagusa moja kwa moja maisha ya watu huku miongoni mwa mazingira bora ya uwekezaji ni uchumi imara, hali ya utulivu, uwepo wa amani, sheria rafiki zinazotumika ili kufanya maamuzi ya haraka. Pia, Dkt. Mpango ametumia fursa hiyo kuwataka wadau wa madini waendelee kufuata sheria ili kuepuka usumbufu mbalimbali ikiwemo kufutiwa leseni za madini. Akizungumzia mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa amesema umeongezeka kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017 hadi asilimia asilimia 9.1 mwaka 2022. “Mwenendo huo unatupa matumaini kwamba Sekta ya Madini itaweza kuchangia hadi asilimia 10 kwenye Pato la Taifa kama ilivyotarajiwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025,” amesema Dkt. Mpango. Amesema suala hilo litafanikiwa endapo Serikali pamoja na wadau wote wa madini watashirikiana kutumia maarifa na ujuzi wa kisasa katika kushiriki shughuli zote za madini kuanzia hatua ya utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji, uongezaji thamani na biashara ya madini. Kwa upande wake, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema Serikali kwa kutambua manufaa ya Sekta ya Madini katika kuchangia uchumi na maendeleo ya nchi, katika Mwaka wa Fedha 2024/25, Bajeti ya Wizara imeongezeka kutoka shilingi bilioni 89 hadi bilioni 231 huku bajeti kubwa ya fedha ikitengwa kwa ajili ya shughuli za utafiti wa madini ili kuiwezesha Serikali kupata taarifa sahihi za kiasi cha madini kilichopo nchini. ‘’ Mhe. mgeni rasmi, mpaka sasa nchi yetu imefanyiwa utafiti wa kina kwa asilimia 16 tu lakini yapo manufaa mengi ya kiuchumi na maendeleo ambayo yametokana na Sekta ya Madini kwa nchi yetu kutokana na utafiti wa madini uliofanywa kutoka katika eneo hilo la asilimia 16,’’ amesisitiza Waziri Mavunde. Waziri Mavunde amebainisha baadhi ya manufaa hayo kuwa ni pamoja na Sekta ya Madini kuchangia asilimia 54 ya fedha za kigeni zinazotokana na mauzo ya bidhaa za madini nje ya nchi na kuongeza kwamba, mapato ya kodi za ndani yanayotokana na madini yameongezeka kufikia shilingi tirilioni 2.1 sawa na asilimia 15. Katika kuhakikisha kwamba shughuli za utafiti wa kina zinafanyika kama ilivyopangwa na kuleta matokeo makubwa, amesema katika mwaka wa fedha 2024/25 Wizara imepanga kununua Helcopter itakayotumika katika shughuli za utafiti wa madini ya kina na ikiwemo ujenzi wa maabara kubwa ya madini katika jiji la Dodoma. Ameongeza kwamba, licha ya utafiti wa kina kutarajia kuinua sekta ya madini, pia itazinufaisha sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo kilimo, maji na afya na kusema ‘’ tukikamilisha utafiti sekta ya kilimo itanufaika sana kutokana na gharama kubwa zinazotumika kuagiza mbolea nje ya nchi ambapo zaidi ya bilioni 650 hutumika kuagiza mbolea nje,’’ amesema mavunde. Awali, akizungumza katika ufunguzi huo, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) John Bina ameipongeza Serikali kutokana na kuendelea kuweka mazingira wezeshi katika sekta ya madini hali ambayo imepelekea kuongezeka kwa uwekezaji unaotokana na shughuli za uchimbaji mdogo, kuongezeka kwa wanunuzi wa madini na kupongeza kuhusu uwepo wa masoko ya madini ambayo yameongeza uwanda mpana wa kuuza madini kwa bei nzuri ikiwemo kuongezeka kwa wanawake wachimbaji wanaomiliki migodi yao. Pia, ametumia fursa hiyo kuipongeza Wizara kwa kufuta leseni za madini sizizoendelezwa na kuiomba Serikali kutoa nafasi kwa wachimbaji wadogo kupatiwa maeneo hayo ili kuyaendeleza kwa ajili ya shughuli za uchimbaji ili hatimaye kuongeza manufaa ya sekta ya madini nchini. Aidha, Bina amemweleza Dkt Mpango kuwa matarajio ya uwepo wa kongamano hilo ni kutoka na matokeo mazuri ikiwemo kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia za kisasa, kuongezeka kwa ajira zinazotokana na shughuli za uchimbaji mdogo, serikali kuzifanyia kazi changamoto za wachimbaji, kujengewa uelewa katika masuala yanayohusu sheria, utunzaji wa mazingira na matumizi bora ya zebaki katika shughuli za uchenjuaji na masuala mengine muhimu. Kongamano la wachimbaji lililoanza leo Juni 20, 2024 linaambatana na maonesho ya madini na vifaa vya uchimbaji, mkutano wa FEMATA ambapo pia kunatarajiwa kufanyika onesho la Madini. Mkutano na maonesho hayo unabebwa na kaulimbiu isemayo Amani iliyopo nchini inapaswa kuleta uchumi imara kupitia soko la madini la Afrika na nchini Tanzania