TUME YA MADINI

Taifa logo iliiyopitishwa

CONTACT US | FAQs | STAFF MAIL | ENGLISH / SWAHILI

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

MINISTRY OF MINERALS

 THE MINING COMMISSION

mwanahamisi.msangi

MAHIMBALI AIAGIZA TUME YA MADINI KUONGEZA KASI YA KUTATUA MIGOGORO

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali ameiagiza Tume ya Madini chini ya Katibu Mtendaji wake, Mhandisi Yahya Samamba kuongeza kasi ya kutatua migogoro ya wachimbaji wa madini nchini. Mahimbali ametoa maelekezo hayo leo Juni 27, 2024 alipotembelea Banda la Tume ya Madini katika Maonesho ya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) yanayoendelea katika Viwanja vya Jakaya Convention Centre (JKCC) jijini Dodoma. Amesema, Tume inafanya kazi nzuri ya kukusanya maduhuli, mapato yameongezeka na yanaonekana na kuitaka iongeze kasi ya kutatua changamoto za wachimbaji wadogo wa madini kwa kuwa wanachangia asilimia 40 ya mapato katika Sekta ya Madini ” Msi -ignore wachimbaji wadogo, STAMICO hata kama ni walezi na nyie Tume mna ‘role’ yenu, ” amesema Mahimbali

MARUFUKU KUWEKA TOZO ZISIZOENDANA NA SHERIA YA MADINI – DKT. KIRUSWA

SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imepiga marufuku Halmashauri kutoza tozo kwa Wachimbaji ambazo zipo kinyume na Sheria mama huku kliniki ya kutibu changamoto za wachimbaji wa madini ikipangwa kuanza Julai 3 2024, nchi nzima. Akizungumza leo Juni 26, 2024 katika Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa, amesema tozo yoyote inayoangukia kwenye Sekta ya Madini ni lazima ioane na Sheria mama. “Ni marufuku na hili ni agizo kwa halmashauri zote nchi nzima, kutoza tozo ambazo ni kinyume na sheria mama, tozo zote zioane na haziwezi kuwa juu ya sheria mama, ili sheria iweze kuwasaidia wachimba madini ni lazima ifanyiwe mapitio. “Sisi kupitia maelekezo ya mama yetu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alishaelekeza sheria na Wizara zote kuhakikisha zinasomana, tupo kwenye mchakato na wenzetu wa TAMISEMI kuzipitia, kubainisha sheria zao na ‘bylaw’ zao ambazo zinaingilia sekta yetu, zinakwaza wawekezaji katika sekta ya madini,” amesema Dkt. Kiruswa. Aidha, Dkt. Kiruswa amesema Wizara itaanza kliniki kuanzia Julai 3, 2024 ya kusikiliza na kutatua changamoto za wadau wa sekta ya madini kwa kushirikiana na Waziri wa Madini Mh Anthony Mavunde, na kusema “Kliniki hii ni mahususi tukifika‘site’ changamoto ambazo Wizara tutaweza kuzitatua hapo kwa hapo tutafanya hivyo, za kisheria na kimifumo tutakwenda kushirikisha wadau husika.”amesisitiza Dkt. Kiruswa. Pia, amesema Wizara ipo kwenye mchakato wa kufanya marekebisho ya Kanuni mbali mbali za sekta ya madini na kueleza kwamba katika bajeti ijayo ya Mwaka wa Fedha 2024/25 kiasi kikubwa cha bajeti kimeelezwa katika shughuli za utafiti huku tafiti hizo zikiwalenga wachimbaji wadogo ili wachimbe kwa tija. “Tafiti zitatusaidia kujua madini tuliyonayo, aina tulizanazo, sehemu yalipo, ubora wake na pale tunapogawa zile leseni mtu anapoomba leseni hata iwe dndogo apewe leseni ambayo tayari taarifa za Stamico zipo,’’ amesema Dkt. Kiruswa. Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa ameiagiza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)) kutoa ripoti ya utafiti kwa umma na sio kuzifungia kwenye makabati. Vilevile, Dkt Kiruswa amesema, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa wachimbaji na kutoa rai kwa wachimbaji kutoa ushirikiano katika maeneo matatu, ikiwemo kuendelea kuwa vinara wa kutii na kufuata sheria ya Madini na Kanuni zake. Sambamba na hilo, Dkt. Kiruswa amewataka wachimbaji kuwa mabalozi wa mfano wa kufuata taratibu na kupambana na utoroshwaji wa madini na kuwataka kuzuia madini kutoroshwa kwa sababu yanavyotoroshwa yanalikosesha taifa mapato huku akiwataka kuendelea kuzitumia taasisi za Wizara kutekeleza majukumu yao. Wakati huo huo, Dkt Kiruswa amezielekeza Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa yote pale wanapokwenda kwenye shughuli zao au mikutano yao wasiende bila kuwa na wawakilishi wa wachimbaji (LEMAS). Kwa upande wake, Rais wa FEMATA John Bina, amewataka wachimbaji wadogo kuipa muda Serikali ili iweze kushughulikia changamoto zao ambazo wameziwasilisha ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali wanachokitaka kwa maslahi ya taifa. “Sisi kama Shirikisho tunaandaa makongamano na mikutano maana yake ni kuishauri Serikali na viongozi kwa sababu sisi ndio wenye sekta kwani huwezi kuwa mwanachama wa FEMATA kama siyo mchimbaji wa madini ili uwe na uchungu na kile unachozungumzia,” amesema Bina. Mkutano wa FEMATA unakwenda sambamba na maonesho ya madini na vifaa vya uchimbaji pamoja na kongamano la wachimbaji

DKT. MPANGO AELEKEZA MADINI YA KIMKAKATI KUWEKEWA MKAZO

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameilekeza Wizara ya Madini na Taasisi zake kuelekeza nguvu katika mikoa yenye madini mkakati ikiwemo Dodoma kufanyiwa utafiti wa kina wa haraka ili kufikia asilimia 50 kabla ya mwaka 2030. Dkt. Mpango ameyasema hayo leo Juni 20, 2024 katika ufunguzi wa Kongamano la Wachimbaji Madini wakati akitembelea mabanda ya maonesho yanayokwenda sambamba na mkutano wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) lililoanza leo hadi Juni 27 katika viwanja vya Jakaya Kikwete Conventional Centre (JKCC) mkoani Dodoma. Amesema kwamba mkakati wa Wizara kupitia vision 2030: yenye kauli mbiu ya madini ni maisha na utajiri itachukua muda mrefu na kwamba miaka sita kutoka sasa ni mingi na kuagiza utafiti huo ufanyike haraka. Kwa sasa utafiti wa kina uliofanyika kwa nchi nzima ni asilimia 16 na malengo ya vision 2030 ni kufikia angalau asilimia 50 ifikapo mwaka huo. Akizungumzia mazingira ya uwekezaji Dkt. Mpango amesema, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara ya Madini kwa wachimbaji wadogo ambapo sasa idadi ya vituo vya ununuzi wa madini imefikia 100 na masoko ya madini 42. Ameongeza kuwa, uchimbaji mdogo wa madini unagusa moja kwa moja maisha ya watu huku miongoni mwa mazingira bora ya uwekezaji ni uchumi imara, hali ya utulivu, uwepo wa amani, sheria rafiki zinazotumika ili kufanya maamuzi ya haraka. Pia, Dkt. Mpango ametumia fursa hiyo kuwataka wadau wa madini waendelee kufuata sheria ili kuepuka usumbufu mbalimbali ikiwemo kufutiwa leseni za madini. Akizungumzia mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa amesema umeongezeka kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017 hadi asilimia asilimia 9.1 mwaka 2022. “Mwenendo huo unatupa matumaini kwamba Sekta ya Madini itaweza kuchangia hadi asilimia 10 kwenye Pato la Taifa kama ilivyotarajiwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025,” amesema Dkt. Mpango. Amesema suala hilo litafanikiwa endapo Serikali pamoja na wadau wote wa madini watashirikiana kutumia maarifa na ujuzi wa kisasa katika kushiriki shughuli zote za madini kuanzia hatua ya utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji, uongezaji thamani na biashara ya madini. Kwa upande wake, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesema Serikali kwa kutambua manufaa ya Sekta ya Madini katika kuchangia uchumi na maendeleo ya nchi, katika Mwaka wa Fedha 2024/25, Bajeti ya Wizara imeongezeka kutoka shilingi bilioni 89 hadi bilioni 231 huku bajeti kubwa ya fedha ikitengwa kwa ajili ya shughuli za utafiti wa madini ili kuiwezesha Serikali kupata taarifa sahihi za kiasi cha madini kilichopo nchini. ‘’ Mhe. mgeni rasmi, mpaka sasa nchi yetu imefanyiwa utafiti wa kina kwa asilimia 16 tu lakini yapo manufaa mengi ya kiuchumi na maendeleo ambayo yametokana na Sekta ya Madini kwa nchi yetu kutokana na utafiti wa madini uliofanywa kutoka katika eneo hilo la asilimia 16,’’ amesisitiza Waziri Mavunde. Waziri Mavunde amebainisha baadhi ya manufaa hayo kuwa ni pamoja na Sekta ya Madini kuchangia asilimia 54 ya fedha za kigeni zinazotokana na mauzo ya bidhaa za madini nje ya nchi na kuongeza kwamba, mapato ya kodi za ndani yanayotokana na madini yameongezeka kufikia shilingi tirilioni 2.1 sawa na asilimia 15. Katika kuhakikisha kwamba shughuli za utafiti wa kina zinafanyika kama ilivyopangwa na kuleta matokeo makubwa, amesema katika mwaka wa fedha 2024/25 Wizara imepanga kununua Helcopter itakayotumika katika shughuli za utafiti wa madini ya kina na ikiwemo ujenzi wa maabara kubwa ya madini katika jiji la Dodoma. Ameongeza kwamba, licha ya utafiti wa kina kutarajia kuinua sekta ya madini, pia itazinufaisha sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo kilimo, maji na afya na kusema ‘’ tukikamilisha utafiti sekta ya kilimo itanufaika sana kutokana na gharama kubwa zinazotumika kuagiza mbolea nje ya nchi ambapo zaidi ya bilioni 650 hutumika kuagiza mbolea nje,’’ amesema mavunde. Awali, akizungumza katika ufunguzi huo, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) John Bina ameipongeza Serikali kutokana na kuendelea kuweka mazingira wezeshi katika sekta ya madini hali ambayo imepelekea kuongezeka kwa uwekezaji unaotokana na shughuli za uchimbaji mdogo, kuongezeka kwa wanunuzi wa madini na kupongeza kuhusu uwepo wa masoko ya madini ambayo yameongeza uwanda mpana wa kuuza madini kwa bei nzuri ikiwemo kuongezeka kwa wanawake wachimbaji wanaomiliki migodi yao. Pia, ametumia fursa hiyo kuipongeza Wizara kwa kufuta leseni za madini sizizoendelezwa na kuiomba Serikali kutoa nafasi kwa wachimbaji wadogo kupatiwa maeneo hayo ili kuyaendeleza kwa ajili ya shughuli za uchimbaji ili hatimaye kuongeza manufaa ya sekta ya madini nchini. Aidha, Bina amemweleza Dkt Mpango kuwa matarajio ya uwepo wa kongamano hilo ni kutoka na matokeo mazuri ikiwemo kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia za kisasa, kuongezeka kwa ajira zinazotokana na shughuli za uchimbaji mdogo, serikali kuzifanyia kazi changamoto za wachimbaji, kujengewa uelewa katika masuala yanayohusu sheria, utunzaji wa mazingira na matumizi bora ya zebaki katika shughuli za uchenjuaji na masuala mengine muhimu. Kongamano la wachimbaji lililoanza leo Juni 20, 2024 linaambatana na maonesho ya madini na vifaa vya uchimbaji, mkutano wa FEMATA ambapo pia kunatarajiwa kufanyika onesho la Madini. Mkutano na maonesho hayo unabebwa na kaulimbiu isemayo Amani iliyopo nchini inapaswa kuleta uchumi imara kupitia soko la madini la Afrika na nchini Tanzania

WAZIRI MAVUNDE AZINDUA TIMU YA KUANDAA ANDIKO LA VISION 2030

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amezindua Timu itakayoandaa Andiko la maudhui ya Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri katika hafla iliyofanyika Juni 12, 2024 jijini Dodoma. Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mavunde amesema kuandaliwa kwa andiko hilo ni matokeo ya maelekezo aliyoyatoa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt. Samia Suluhu ya kufanyika kwa utafiti wa kina ili kuboresha eneo hilo na hatimaye kuwawezesha watanzania wasichimbe kwa kubahatisha. Waziri Mavunde ameongeza kwamba, mpaka sasa utafiti wa kina kwa nchi nzima umefanyika kwa asilimia 16 ambapo mpango uliopo kupitia Vision 2030 ni kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030. ‘’ Tanzania imejaliwa kuwa na madini mbalimbali lakini bado hatuna uwezo mkubwa wa kubaini kiwango cha madini hayo. Kupitia vision 2030 tutabaini yote hayo,’’ amesema Waziri Mavunde. Akizungumzia kuhusu sekta zitakazo nufaika na utekelezaji wa Vision 2030, amezitaja kuwa ni pamoja na sekta ya Kilimo , Afya , Maji na Viwanda na kuongeza kwamba lengo ni kuhakikisha Sekta ya madini inajifunganisha na sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo kuziwezesha kukua. ‘’ Hekta milioni 3.6 zimeathirika na tindikali kufanya shughuli za kilimo kuwa ngumu, tukifanya utafiti wa kina utasaidia eneo kubwa la nchi yetu. Tunaona sekta ya madini ina mchango mkubwa wa kuendeleza sekta nyingine, amesisitiza Waziri Mavunde. Pia, Waziri Mavunde ametaja baadhi ya manufaa yaliyotokana na matokeo ya utafiti wa kina uliofanywa kwa asilimia 16 nchi nzima na kubainisha kuwa ni pamoja na kuiwezesha Sekta ya Madini kuongoza kwa kuchangia fedha za kigeni kutokana na mauzo ya bidhaa za madini nje ya nchi ambapo mchango wake umefikia asilimia 56, kuongezeka kwa mapato ya ndani yanayotokana na sekta ya kufikia asilimia 15. Katika hatua nyingine, Waziri Madini ameikabidhi Kamati hiyo inayoongozwa na Prof. AbdulKarim Mruma hadidu 14 za rejea zitakazowezesha kuandaliwa kwa andiko hilo na kuitaka kuhakikisha andiko hilo linawezesha utekelezaji wa vision 2030 kutoka na matokeo makubwa nane ikiwemo kusaidia kuongeza mchango wa Sekta ya madini kwenye pato la taifa, kuwezesha upatikanaji wa fedha za kigeni, kuwezesha maendeleo ya viwanda na sekta nyingine na kuwezesha ushiriki wa watanzania katika sekta ya madini. Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameipongeza Wizara ya Madini kwa kufanya utafiti wa awali Mkoani Dodoma ulionesha uwepo wa aina mbalimbali za madini na kuiomba Wizara kuendelea na utafiti wa kina ili kujua kiasi cha mashapo yaliyopo. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini Dkt. Mathayo David Mathayo amesema kuwa Vision 2030 itaongeza wigo mpana kwa watanzania kushiriki katika mnyororo unaounganisha sekta nzima ya madini pamoja na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya wizara likiwemo Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST). Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa ameipongeza Wizara ya Madini kuja na Vision 2030 akisisitiza kuwa umefika muda wananchi kunufaika na rasilimali madini. Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Madini, amesema kuwa wizara ipo tayari kusimamia maono Vision 2030 ambayo yataleta mabadiliko makubwa ya kisekta kwa miaka sita ijayo kupitia hadidu za rejea kama zilivyoainishwa. #VISION 2030: Madini ni Maisha na Utajiri

TUME YA MADINI YAJIPANGA KUKUSANYA SHILINGI TRILIONI 1

Wakati Bajeti Kuu ya Serikali ikitarajiwa kuwasilishwa kesho, Menejimenti ya Tume ya Madini imetakiwa kufanya kazi kwa weledi, umoja na mshikamano ili kufikia lengo la Serikali la makusanyo ya shilingi Trilioni moja kutoka Sekta ya Madini kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Hayo yamesemwa leo Juni 12, 2024 na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba katika ufunguzi wa kikao cha Menejimenti ya Tume ya Madini jijini Tanga chenye lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa mwaka 2023/2024 na kuweka mikakati thabiti ya utekelezaji kwa mwaka 2024/2025. Amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Juni 12, 2024 Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya shilingi Bilioni 703.94 sawa na asilimia 79.80 ya lengo walilowekewa la kukusanya kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambalo ni shilingi Bilioni 882.12. “Kwa mwaka wa fedha unaoisha tumeenda vizuri kwenye makusanyo, haijawahi kutokea, hata hivyo tunapaswa kukaza msuli zaidi ili kufikia lengo la makusanyo ya Serikali tulilopangiwa la kukusanya Shilingi Trilioni moja, kupitia Sekta ya Madini kwa mwaka mpya wa fedha unaoanza Julai 2024/2025” amesema Mhandisi Samamba. Aidha, ameitaka Menejimenti ya Tume itoke na mikakati madhubuti ya kuhakikisha inaziba mianya ya upotevu wa mapato. “Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuweni wakali kuhakikisha mnaziba mianya yote inayokwamisha ukusanyaji mapato ili shida inapotokea kwenye mkoa wako usije kuwajibishwa kwa kushindwa kusimamia vyema ukusanyaji wa mapato,”amesema Mhandisi Samamba. Pia, Mhandisi Samamba amezitaka Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa ambazo zimeshindwa kufikia lengo kwa mwaka huu unaoisha, zijipange vyema kwa kipindi kilichobaki na mwaka ujao 2024/2025 na kuwataka kuwa wabunifu zaidi ili kuongeza ufanisi kazini bila kusahau kuboresha mazingira ya utendaji kazi na kusimamia maslahi ya watumishi. “Tunapaswa kuhakikisha kuwa katika Ofisi tunazozisimamia kunakuwa na hali ya usawa, ushirikiano na maelewano baina ya watumishi kwa ngazi zote,umoja, na ushirikiano ndio iwe nguzo yetu ili kufikia lengo tulilowekewa,” amesisitiza Mhandisi Samamba

KURUGENZI YA UKAGUZI NA BIASHARA YA MADINI KUENDELEA KUJENGEWA UWEZO

Akifungua kikao kazi cha kuwajengea uwezo Watumishi wa Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini Mkoani Morogoro Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Andrew Mgaya amesema lengo ni kukutana ili kujengeana uwezo ili kuwa wabunifu katika kuongeza makusanyo na kufikia lengo la shilingi bilioni 999 kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Amesema nia ya kuwepo kwa kikao hiki ni kuboresha utendaji kazi wa Idara pamoja na kujengeana uwezo katika masuala mbalimbali hasa utekelezaji wa mpango kazi wa sehemu kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na mpango kazi kwa mwaka 2024/2025. “Kikao hiki kiwe ni chachu ya kufika mbali ki Idara tuwajibike katika kazi zetu, tushirikiane kwa pamoja na kufanya kazi kwa weledi ili tufikie lengo tulilojiwekea ,”amesema Mgaya. Pia, amewaomba Watumishi wa Idara ya Ukaguzi na Biashara ya Madini kusikiliza kwa umakini mada na mafunzo ili kuleta matokeo chanya kwa mwaka ujao wa fedha.

MKOA WA KIMADINI CHUNYA WAKUSANYA ZAIDI YA BILIONI 30

Mkoa wa kimadini Chunya mpaka kufikia Juni 7, 2024 umefanikiwa kukusanya maduhuli ya Shilingi bilioni 34.9 katika mnyororo wa uchimbaji madini. Hayo yamebainishwa leo Juni 7, 2024 na Afisa Madini Mkazi (RMO) mkoa wa kimadini Chunya Mha.Laurent Mayala wakati akiwasilisha taarifa ya mwenendo wa sekta ya Madini wilayani Chunya kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Kheri Mahimbali. Mha.Mayala amesema kuwa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 Ofisi imefanikiwa kudhibiti matukio ya utorosha madini ambapo mpaka sasa kiasi cha gramu 8,189.79 za madini ya dhahabu zimekamatwa. Akielezea kuhusu mwenendo wa utoaji leseni za ununuzi mdogo na mkubwa wa madini , Mha.Mayala amesema kuwa , idadi ya leseni 65 zimetolewa kwa wanunuzi wakubwa wa madini na leseni 315 za wanunuzi wadogo. Akifafanua juu ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo wilayani Chunya Mha.Mayala amesema kuwa tayari wametenga maeneo mbalimbali ikiwemo Makongolosi , Mawelo,Sagambi, Matundasi na Kasisi kwa ajili ya kurasimishwa kwa wachimbaji wadogo ili kukuza shughuli zao za uchimbaji. Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali ameipongeza Ofisi ya Madini Wilayani Chunya kwa kufanya vizuri katika usimamizi mzuri wa shughuli zote zinazohusiana na sekta ya madini. Mahimbali ameongeza kuwa mkoa wa Kimadini Chunya ni mmoja wa mkoa muhimu sana katika sekta ya madini hivyo amewaataka watumishi kuendelea kufanya kazi kwa weledi , ushirikiano na kuongeza ubunifu ili kuendelea kufikia malengo yaliyowekwa. Ziara hii ya siku mbili wilayani Chunya Mahimbali ameambatana na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Madini kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali za uchimbaji , uzalisha na uchenjuaji katika mnyororo mzima wa sekta ya madini

KIKOSI KAZI KUUNDWA KUDHIBITI UTOROSHAJI WA MADINI MKOANI SONGWE

TUME ya Madini Mkoa wa Songwe imeunda kikosi kazi maalum cha kupambana na kudhibiti utoroshaji wa madini na kusababisha serikali kukosa mapato. Hayo yamesemwa na Afisa Madini Mkazi – Songwe, Chone Malembo wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwatembelea wachimbaji wadogo katika eneo la Mbangala lililopo mkoani humo. “Kwa sasa kuna mawasiliano ambayo yanaendelea tunataka kutengeneza kikosi kazi madini Mkoa ambacho kazi yake itakuwa ni kufanya uchunguzi na kutoa taarifa kuhusu utoroshaji madini mahali husika ili kuchukua hatua stahiki lengo ni kudhibiti utoroshaji ambao husababisha Serikali kukosa mapato,”amesema Chone. Katika hatua nyingine, Afisa huyo amesema wamegundua madini mapya aina ya Solidite ambayo yanapatikana Wilaya ya Momba.    

Scroll to Top