• Tume ya Madini yaainisha mikakati yake kufikia 10% ya Pato la Taifa • Yasimamia ajira 18,853 za Watanzania katika kampuni za madini • Leseni za madini 34,000 zatolewa • Katibu Mtendaji aipongeza Wizara ya Madini chini ya Waziri Mavunde kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini. Mwandishi Maalum, Tume ya Madini. MIAKA mitatu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan madarakani, Tume ya Madini imeainisha mafanikio yake ikiwemo ongezeko la ukusanyaji wa maduhuli, kuongezeka kwa usimamizi kwenye biashara ya madini na ukaguzi wa migodi na mazingira sambamba na ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini. Akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya Habari, leo Oktoba 24, 2024 katika ukumbi wa Chuo cha Utalii jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo amesema kupitia usimamizi unaofanywa na Tume ya Madini, kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya Serikali kimepanda kutoka Shilingi bilioni 624.61 zilizokusanywa Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi kufikia Shilingi bilioni 753.82 Mwaka wa Fedha 2023/2024, makusanyo hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.7 ya makusanyo kwa miaka mitatu. “Mathalan katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo tulipewa lengo la kukusanya shilingi Trilioni Moja, hadi kufikia Oktoba 21, 2024 Tume ya Madini imefanikiwa kukusanya Jumla ya Shilingi bilioni 312.75 sawa na asilimia 31.28 ya lengo la mwaka,”amesema Mhandisi Lwamo. Amesema, mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.2 Mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 9.0 Mwaka 2023 hiyo ni kutokana na kuimarika kwa usimamizi wa shughuli mbalimbali za madini nchini. Mhandisi Lwamo amesema vilevile, ukuaji wa Sekta ya Madini umeongezeka kutoka asilimia 9.4 Mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 11.3 Mwaka 2023 kutokana na kuendelea kuimarika kwa Sekta, Mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa utaongezeka na kufikia asilimia 10 au zaidi ifikapo Mwaka 2025 kama ilivyoelezwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. Amesema, katika kipindi rejewa, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini kwa kushirikiana na Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini iliendelea kusimamia utendaji kazi wa Masoko ya Madini na vituo vya ununuzi wa Madini nchini. “Katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 mauzo ya madini katika Masoko na Vituo vya Ununuzi wa madini yalikua Shilingi bilioni 2,592.02 na mapato yaliyopatikana kutokana na mauzo hayo ni kiasi cha Shilingi bilioni 180.13 ikilinganishwa na Mwaka wa Fedha 2021/2022 ambapo ilikua Shilingi bilioni 2,361.80 na mapato ya Serikali yaliyopatikana ni Shilingi bilioni 164.09 ambapo mapato hayo yalihusisha mrabaha na ada ya ukaguzi wa madini nchini,”amesema Mhandisi Lwamo. Aidha, Mhandisi Lwamo ameweka wazi uelekeo wa Sekta ya Madini katika kuchangia Pato la Taifa ili kufikia asilimia 10 au zaidi ifikapo mwaka 2025 kama inavyofafanuliwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 pamoja na Mpango Mkakati wa Tume ya Madini wa Mwaka 2024/2025, 2025/2026. Mhandisi Lwamo amesema, katika kuhakikisha azma hiyo inafikiwa, Tume ya Madini imeweka mikakati endelevu ikiwemo kuimarisha usimamizi na udhibiti katika maeneo ya uzalishaji wa madini ujenzi na madini ya viwandani kwa kuongeza Wakaguzi Wasaidizi wa Madini Ujenzi (AMAs), vitendea kazi (PoS) pamoja na kushirikisha Mamlaka nyingine za Serikali zinazosimamia na kutumia rasilimali hizi (Halmashauri, Polisi, TARURA na TANROADS) na kuongeza kuwa, lengo ni kuongezeka kwa makusanyo yatokanayo na rasilimali ya madini ujenzi na madini ya viwandani. Pia, amesema mkakati mwingine ni kuimarisha udhibiti wa biashara haramu ya madini hususani utoroshaji wa madini kwa kuhamasisha umuhimu wa kutumia Masoko na vituo vya madini nchini; kuimarisha vituo vya ukaguzi (exit-points) katika maeneo ya mipakani, bandarini pamoja na viwanja vya ndege lengo likiwa ni kupunguza matukio ya utoroshaji wa madini na hivyo kuwezesha Serikali kupata takwimu sahihi na mapato stahiki. “Uboreshaji na Usimamizi thabiti wa Mfumo wa Utoaji wa Leseni za madini, matokeo ni kupunguza migogoro itokanayo na mwingiliano wa maombi ya leseni, kupunguza muda wa utoaji huduma pamoja na kuongeza idadi ya leseni zitakazotolewa kwa mwaka hivyo kuhamasisha uwekezaji,”amesema Mhandisi Lwamo. Amesema, mkakati mwingine ni kuimarisha ukaguzi katika shughuli za uchimbaji katika migodi kwa lengo la kuwa na uchimbaji endelevu unaozingatia usalama, afya na mazingira, lengo kuongeza mapato, kuimarisha uchimbaji endelevu unaojali mazingira kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo. “ Pia, kuimarisha Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa (RMOs) na Maabara katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji hapa nchini, lengo likiwa ni kusogeza huduma karibu na wadau hivyo kuchochea uwekezaji utakaowezesha Serikali kuongeza mapato yatokanayo na rasilimali madini” amesisitiza Mhandisi Lwamo. Ameendelea kueleza mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuimarisha shughuli za tafiti zinazohusiana na utambuzi wa vyanzo vipya vya mapato yatokanayo na rasilimali za madini, lengo likiwa ni kuiwezesha Taasisi kuongeza wigo wa makusanyo yatokanayo na rasilimali madini ikiwemo kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwa wachimbaji wa madini ili kuongeza mapato, ajira na kuwa Sekta endelevu. Amesema, Tume ya Madini katika kuhakikisha kuwa Wananchi wananufaika na rasilimali madini, imeendelea kusimamia uwasilishaji wa Mipango ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCPs) kutoka kwa Wamiliki na Waombaji wa leseni za madini pamoja na watoa huduma kama takwa mojawapo la Sheria ya Madini Sura ya 123. Mhandisi Lwamo amesema, katika kipindi rejewa, jumla ya Mipango 1,050 ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini ilipokelewa na kufanyiwa uchambuzi. Kati ya Mipango iliyowasilishwa, 1,036 ilikidhi vigezo na kuidhinishwa na Mipango 14 haikukidhi vigezo hivyo ilirejeshwa kwa wahusika kwa ajili ya marekebisho. “Aidha Tume ya Madini imeendelea kusimamia kikamilifu upatikanaji wa ajira kwa Watanzania kutoka kwenye Makampuni mbalimbali ya Uchimbaji ambapo katika kipindi rejewa Kampuni ziliweza kuzalisha ajira 19,356 ambapo kati ya hizo 18,853 ni Watanzania sawa na asilimia 97.40 na 503 ni wageni sawa asilimia 2.60 ya ajira zote zilizozalishwa,”amesema Mhandisi Lwamo. Vilevile, amesema jumla ya bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,780,161,183.28 ziliuzwa na kusambazwa migodini ambapo kati ya bidhaa hizo Kampuni za Watanzania zilifanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani (USD) 3,465,592,451.28 sawa na asilimia 91.68 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote na huduma zilizotolewa migodini. Mhandisi Lwamo amesema pia, Tume ya Madini imekuwa ikitoa leseni za uendeshaji wa shughuli za madini kwa wadau wake kwa