TUME YA MADINI

Taifa logo iliiyopitishwa

CONTACT US | FAQs | STAFF MAIL | ENGLISH / SWAHILI

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

MINISTRY OF MINERALS

 THE MINING COMMISSION

WAZIRI MAVUNDE AWATAKA MAAFISA MADINI WAKAZI WA MIKOA KUONGEZA KASI UKUSANYAJI WA MADUHULI

Mwanza

 

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuongeza kasi ya ukusanyaji wa maduhuli ili kufikia lengo lililowekwa na Serikali la kukusanya shilingi bilioni 882 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024

Waziri Mavunde aliyasema hayo Januari 06, 2024 jijini Mwanza kwenye kikao chake na Menejimenti ya Tume ya Madini kilichohusisha Makamishna wa Tume ya Madini, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, Wakurugenzi, Mameneja, Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa chenye lengo la kuweka mikakati ya namna ya kufikia malengo ya utekelezaji katika Sekta ya Madini hususan katika eneo la ukusanyaji wa maduhuli katika kipindi cha nusu mwaka kilichobaki.

Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho walikuwa ni pamoja na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali na Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga.

Akielezea mwenendo wa ukusanyaji wa maduhuli katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024 Waziri Mavunde alisema kuwa kati ya mwezi Julai 2023 hadi Januari 05, 2024 kiasi cha shilingi bilioni 384 kimeshakusanywa na kuwataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu zoezi husika.

Aidha, Waziri Mavunde aliwataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuhakikisha wanasimamia leseni zinazotolewa kwa kuhakikisha zinafanyiwa kazi na kufuta zisizofanyiwa kazi kwa kufuata taratibu za kisheria.

Katika hatua nyingine, aliwataka maafisa madini wakazi wa mikoa kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama kwenye udhibiti wa utoroshaji wa madini.

Pia, aliwataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuwa mstari wa mbele kuwasaidia wachimbaji wa madini kwenye shughuli zao na kuwa mstari wa mbele kwenye utatuzi wa changamoto badala ya kusubiri zifike Wizarani.

Sambamba na kuwataka maafisa madini wakazi wa mikoa kufanya kazi kidigitali na ubunifu wa hali ya juu, Waziri Mavunde aliwataka kufanya kazi kwa kufuata sheria na kanuni kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini.

Naye Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa aliongeza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto zinazowakumba wadau wa madini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miundombinu ya umeme na barabara inaboreshwa kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.

Katika hatua nyingine, Dkt Kiruswa aliwataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuwaelekeza wawekezaji wanaopatiwa leseni za madini kuomba ridhaa kwa wananchi wa maeneo husika kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji wa madini sambamba na kuboresha huduma za jamii (CSR) na kutoa kipaumbele cha huduma na ajira kwa wakazi wa maeneo husika.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali alisisitiza kuwa Wizara imejipanga kuboresha mazingira ya ofisi za maafisa madini wakazi wa mikoa ikiwemo kuongeza rasilimaliwatu pamoja na vifaa.

“Kiu yetu kubwa ni kuona shughuli za uchimbaji wa madini zinaendelea pasipo kuwepo na changamoto yoyote hivyo wananchi kuendelea kunufaika na rasilimali za madini kupitia ajira, huduma na Serikali kupata kodi mbalimbali,” alisema Mahimbali.

Awali akielezea mafanikio katika kikao hicho, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba alieleza kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa kasi ya makusanyo ya maduhuli ambayo yameendelea kuimarika kila mwaka, kupungua kwa migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na kupungua kwa matukio ya utoroshaji wa madini.

“Bado tumeendelea kuweka nguvu katika kuhakikisha miradi mikubwa ya uchimbaji wa madini inaanza mara moja ili mchango wa Sekta ya Madini kwenye uchumi wa nchi uendelee kukua,” alisema Mhandisi Samamba

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top