▪️Wizara ya Madini Yaja na Mkakati wa Uongezaji Thamani Madini kwa Miaka Mitano (2026/27-2030/31)
▪️Dkt. Kiruswa Asisitiza Maonesho ya Madini Geita Kusaidia Uanzishwaji wa Miradi,
▪️Awasihi Washiriki Kujisasili Mapema ili Kushiriki Mkutano wa 7 wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini – TMIC 2026
▪️RC Mnyeti Asisitiza Geita Kuendelea kuwa Kitovu cha Teknolojia ya Madini Tanzania
📍Geita
Serikali imesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia za kisasa na uwekezaji katika kuongeza tija, usalama na thamani ya madini nchini, huku ikiwataka wadau wa sekta hiyo kuwajibika kwa pamoja kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania na kuchangia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, leo Septemba 27, 2026, wakati akifungua rasmi Maonesho ya Tisa ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Bombambili, mkoani Geita na kusema kaulimbiu ya mwaka huu, ”Madini ni Utajiri - Tuwajibike kwa Pamoja Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” inaweka wajibu kwa Serikali, wawekezaji, wachimbaji na wananchi ambapo amewataka wadau wa Sekta ya Madini kuhakikisha Maonesho ya Geita hayabaki kuwa
Dkt. Kiruswa amesisitiza kuwa uwajibikaji huo unahusu matumizi ya teknolojia sahihi, uzingatiaji wa sheria, usalama na afya migodini, na utunzaji wa mazingira na kuhakikisha jamii zinazozunguka maeneo ya uchimbaji zinapata manufaa stahiki na kwamba maonesho hayo yanapaswa kuwa chachu ya kubadilisha maazimio kuwa miradi, ubia na matokeo yanayopimika.
Akizungumzia utafiti, Dkt. Kiruswa amesema Wizara inalenga kupanua utafiti wa kina wa jiofizikia kwa kutumia ndege (High-Resolution Airborne Geophysical Survey). Lengo ni kufikia angalau asilimia 50 ya eneo la nchi ifikapo mwaka 2030, kutoka takribani asilimia 16 ya sasa, na kwamba hatua hiyo itaondoa uchimbaji wa kubahatisha, itapunguza gharama za utafutaji na itawaepusha wachimbaji wadogo kupoteza mitaji yao. Ili kufanikisha azma hiyo, Serikali imetunga Sheria inayoelekeza asilimia 10 ya mapato yatokanayo na shughuli za madini kutengwa kwa ajili ya tafiti za jiosayansi.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imeandaa Mkakati wa Uongezaji Thamani wa Madini wa 2026/27-2030/31. Mkakati huo utaimarisha uchakataji, uchenjuaji na usafishaji wa madini nchini kwa kushirikiana na TISEZA, ili kuongeza ajira na fursa za biashara kwa Watanzania, amezipongeza Kampuni za madini zinazozingatia sheria ya ushirikishwaji wa wazawa na kusema kuwa maboresho ya Sheria hiyo yameongeza idadi ya Kampuni za Kitanzania zinazouza bidhaa na kutoa huduma migodini.
Dkt. Kiruswa amewahimiza vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum kuchangamkia Programu ya Madini kwa Kesho Njema (Mining for a Brighter Tomorrow - MBT). Programu hiyo inatoa fursa za leseni, ushauri wa kitaalamu, taarifa za utafiti na, katika miradi yenye sifa, vifaa na mitambo, "Lengo la Serikali ni kuona makundi haya yanakuwa washiriki wa maendeleo ya sekta, na siyo watazamaji wa maendeleo hayo," amesema Dkt. Kiruswa.
Aidha, amewasihi wadau wa sekta ya madini kujisajili mapema ili kushiriki katika Mkutano wa 7 wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TMIC 2026), akieleza kuwa mkutano huo utatoa fursa kwa wawekezaji, wataalamu na wadau mbalimbali kujenga ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kujadili fursa za uwekezaji katika sekta ya madini nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti, amesema Geita inaendelea kuwa kitovu cha matumizi ya teknolojia za kisasa katika shughuli za madini nchini, akieleza kuwa Maonesho ya Tisa ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini ni sehemu ya mkakati wa kuonesha na kukuza matumizi ya teknolojia hizo katika shughuli za uchimbaji na huduma zinazohusiana na madini na kuwa Sekta ya Madini ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya ajira na maendeleo ya kiuchumi mkoani Geita, hivyo vijana wanapaswa kutumia fursa ya maonesho hayo kujifunza teknolojia, ubunifu na fursa mbalimbali zinazotokana na sekta hiyo ili kujenga uwezo na kushiriki kikamilifu katika shughuli za madini.