THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
MINING COMMISSION

ZAMBIA YASHANGAZWA MFUMO USIMAMIZI SEKTA YA MADINI


news title here
06
Jul
2022

Ujumbe kutoka Serikali ya Zambia ukiongozwa na Waziri wa Madini na Maendeleo ya Migodi Paul Kabuswe umeshangazwa na mfumo wa usimamizi uliopo kwenye sekta ya madini nchini.

Waziri Kabuswe ambaye pia ameongozana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na wataalam wengine wapo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku tatu (3) kujifunza kuhusu usimamizi wa sekta ya madini hususan kwenye shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu zinazofanywa na wachimbaji wadogo.

Ujumbe huo umeelimishwa na Wataalam kutoka Tume ya Madini na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuhusu namna Serikali inavyosimamia shughuli za sekta ya madini kuanzia shughuli za utafiti, uombaji leseni, utoaji leseni, uchimbaji wa madini, uchenjuaji madini, biashara ya madini hususan kwa madini ya dhahabu na taratibu za kusafirisha madini nje ya nchi.

Sekta ya Madini Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kwa nchi nyingi za Afrika kwa namna ilivyoweza kurasimisha sekta ndogo ya uchimbaji madini na hivyo kupelekea wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kupitia mfumo ulio rasmi ambapo Serikali inaweza kufuatilia shughuli zao mpaka hatua ya kuuza madini yao, kupitia katika masoko ya madini 42 na vituo vya ununuzi 75 vilivyoanzishwa nchi nzima huku makusanyo ya serikali kutoka kwa wachimbaji wadogo yakiongezeka.

Hatua hiyo imewezesha mchango wa sekta hiyo ndogo kuchangia kwenye makusanyo ya maduhuli ya Serikali kutoka asilimia 4 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 30 hivi sasa. Aidha, uwepo wa Ofisi 29 za Madini mikoa mbalimbali nchini ambazo zinaratibu shughuli za madini idadi yake imeonesha kumshangaza Waziri huyo na ujumbe wake ikilinganishwa na ofisi 6 za madini zilizopo nchini mwake.

Akizungumza na vyombo vya habari, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema nchi ya Zambia inatarajia kufanya marekebisho ya Sera na Sheria zake za madini hivyo ujumbe huo umefika kujifunza namna wachimbaji wadogo wanavyofanya shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu, namna biashara ya madini ya dhahabu inavyofanyika kupitia masoko ya madini jambo ambalo limefanya mfumo wake kuwa mkubwa na mfano kwa nchi nyingine Afrika na duniani.

Ameongeza kwamba, ili sekta ya Madini ilete manufaa kwa nchi ni muhimu ikasimamiwa kikamilifu kwa kuweka mifumo madhubuti itakayosaidia nchi na watu wake kunufaika na rasilimali madini, kukuza uchumi wa nchi na kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Kwa upande wake, Waziri Kabuswe amesema nchi hizo mbili zimekuwa na uhusiano na ushirikiano wa kipindi kirefu na nchi hiyo imeshuhudia namna uchimbaji mdogo wa madini nchini ulivyofanikiwa hivyo, ujumbe huo umefika kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kusimamia sekta ya madini.

‘‘Tumeona hatunufaiki ipasavyo na sekta ya madini, tunataka watu wetu wapate ajira kwenye nafasi muhimu kupitia sekta hii, tunataka wananchi wanufaike ipasavyo ili vizazi vyetu vijavyo visikute mashimo tu, tunayo madini kama dhahabu, shaba, manganese tunataka madini haya yalete tija kwa sababu tumeona namna Tanzania inavyofanya vizuri sana tumeona ipo haja ya sisi kujifunza na kubadilishana uzoefu,’’ amesema Waziri Kabuswe.

Aidha, kutokana na kupatiwa taarifa muhimu ambazo zimeonekana kuleta mageuzi kwenye sekta ya madini, Waziri Kabuswe ameleeza kuwa, ipo haja kwa wizara yake kuwaleta tena wataalam wake kuja kujifunza kwa kina.