THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
MINING COMMISSION

WAZIRI MAVUNDE AWATAKA MAAFISA MADINI WAKAZI WA MIKOA KUIMARISHA UDHIBITI WA UTOROSHAJI WA MADINI


news title here
26
Sep
2023

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kwa kushirikiana na vyombo vya usalama kuongeza udhibiti wa utoroshaji wa madini sambamba na kufanya kazi kwa kufuata Sheria ya Madini, kanuni zake na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali hivyo Sekta ya Madini kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa na kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Mavunde ameyasema hayo leo Septemba 26, 2023 jijini Mwanza kwenye kikao chake na menejimenti ya Tume ya Madini kilichoshirikisha Wakurugenzi, mameneja na maafisa madini wakazi wa mikoa. Viongozi walioshiriki ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali, Kamishna wa Madini Nchini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Kamishna wa Tume ya Madini, Janet Lekashingo na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba.

Amesema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuweka mikakati mbalimbali ya usimamizi wa Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa udhibiti wa utoroshaji wa madini, maboresho ya mfumo wa usimamizi wa Leseni za Madini, biashara ya madini na kufanya tafiti za madini katika maeneo yote nchini kabla ya mwaka 2030 ikiwa ni utekelezaji wa Dira ya Madini ya Mwaka 2030 ya “Madini ni Maisha na Utajiri.”

“Kwenye suala la utoroshaji wa madini Serikali haitamfumbia macho mfanyabiashara au mtu yeyote atakayebainika anatorosha madini, mkakati ni kuhakikisha madini yote yanauzwa kupitia masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa nchini na Serikali kupata kodi itakayotumika kuboresha Sekta nyingine muhimu,” amesema Mavunde.

Katika hatua nyingine, amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kutatua migogoro kwenye shughuli za uchimbaji wa madini badala ya kusubiri kutatuliwa katika ngazi za juu.

Aidha, amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kufanya kazi kwa kushirikiana kwa upendo na kuongeza kuwa Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto zote katika Sekta ya Madini.

Pia amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kufanya kazi kwa bidii na ubunifu wa hali ya juu na kusisitiza kuwa utendaji wao utapimwa kupitia matokeo yanayoonekana hususan kwenye maeneo ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.

Akielezea mwelekeo wa utekelezaji wa Dira ya Madini ya mwaka 2030 inayosema Madini ni Maisha na Utajiri, Mavunde amesema kuwa Wizara kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imepanga kufanya tafiti katika maeneo yote nchini kabla ya mwaka 2030 na kuongeza kuwa mazungumzo yameshafanyika na kampuni za nje kwa ajili ya kuanza kufanya tafiti mapema kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya upigaji picha kwa kutumia drones na ndege ambapo majaribio yatafanyika katika eneo la mkoa wa Geita na maeneo mengine yatakayobainishwa.

Amefafanua kuwa taarifa za tafiti zitasaidia kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Madini na kuongeza ukusanyaji wa maduhuli sambamba na nchi kuingia kwenye ramani ya dunia kwenye madini ya kimkakati.

“Mahitaji ya madini ya kimkakati duniani kwa sasa ni tani milioni 10, mahitaji yanatarajiwa kuongezeka hadi kufikia tani milioni 150 ifikapo mwaka 2050 ambapo kama nchi tunatakiwa kujipanga haswa kuhakikisha tunakuwa miongoni mwa nchi zenye fursa nyingi za uwekezaji katika madini ya kimkakati,” amesema Waziri Mavunde.

Awali akizungumza kwenye kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali sambamba na kupongeza uteuzi wa Waziri Mavunde uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Wizara na Taasisi zake itaendelea kumpa ushirikiano katika kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa miongoni mwa Sekta zinazoongoza kwenye mchango mkubwa katikaukuaji wa uchumi wa nchi.