WAFANYABISHARA WA MADINI WATAKIWA KUEPUKA UTOROSHAJI NA BIASHARA HARAMU YA MADINI

Mar
2023
Kamishna wa Tume wa Madini Profesa. Abdulkarim Mruma ametaka Wafanyabiashara wa madini nchini kuepuka na vitendo vya utoroshaji na biashara haramu ya madini, kwani vitendo hivyo vina athari kwa Wafanyabishara na Taifa kwa ujumla.
Profesa. Mruma ameyasema hayo Februari 27, 2023 kwenye ufunguzi wa mafunzo kwa Wafanyabiashara wakubwa wa madini kutoka mikoa ya Geita, Kahama, Mara, Mwanza, Mbogwe, Shinyanga, Simiyu, na Singida, juu ya masuala ya biashara ya madini pamoja na mafanikio na changamoto za shughuli za biashara ya madini hapa nchini, yaliyofanyika katika ukumbi wa maji house mkoani Mwanza ambayo yamekutanisha Wakurugenzi, Mameneja na Watumishi wa Tume ya Madini, Maafisa Madini Wakazi wa mikoa ya Geita, Mwanza, Kahama, Mara, Mbogwe, Shinyanga, Simiyu na Singida, Viongozi na Wafanyabiashara Wakubwa wa madini.
Profesa Mruma amesema kuwa mafunzo haya ya siku mbili yanalenga kuhakikisha kuwa shughuli za biashara ya madini zinafanyika kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali iliyowekwa pamoja na kufanya biashara ya madini iwe na faida na tija kwa Washiriki pamoja na Taifa kwa ujumla.
"Wote tunatambua kuwa shughuli ya biashara ya madini ina manufaa kwenu, ikiwa ni mapato kwa Wafanyabishara wa madini, Wachimbaji wa madini, fursa za ajira pamoja na kutangaza rasilimali za Taifa letu duniani kote kwa lengo la kuvutia wawekezaji," amesema Profesa Mruma.
Profesa Mruma amesema kuwa mafunzo haya yatazingatia pia utaratibu wa utoaji leseni za biashara ya madini, Sheria zinazohusu biashara ya madini pamoja na usimamizi wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini.
"Pamoja na mafanikio hayo, nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikija hapa nchini kwetu kujifunza namna tunavyoendesha masoko ya madini, hii ni kutokana na ushirikiano mkubwa mnaoipatia Wizara ya Madini na nchi kwa ujumla kwa mwitikio wenu wa kufanya biasahara katika masoko ya madini," amesema Profesa Mruma.
Profesa Mruma amesema kuwa kupitia mafunzo haya kama Wafanyabiashara wa madini mna jukumu la kufanya shughuli zenu kwa weledi, kujifunza, kuuliza maswali na kupata ufumbuzi wa changamoto zinazotukabili ili kuongeza uelewa na kukuza tija katika shughuli za biashara ya madini.