WACHIMBAJI MZINGATIE USALAMA NA MAZINGIRA MIGODINI

Jan
2023
Mwenyekiti wa Tume wa Madini Prof. Idris Kikula amesema shughuli za uchimbaji wa madini nchini zinaambatana na uharibifu wa mazingira pamoja na masuala ya afya na Usalama , hivyo kila mchimbaji anawajibu wa kusimamia mazingira kwa mujibu wa Sheria.
Prof. Kikula ameyasema hayo Januari 27, 2023 kwenye ufunguzi wa mafunzo kuhusu Usalama, Afya,Usimamizi wa Mazingira na matumizi salama ya baruti migodini kwa Wachimbaji wadogo wa madini, yaliyofanyika katika ukumbi wa Rhoma mkoani Singida ambayo yamekutanisha Maafisa Madini Wakazi wa mikoa ya Singida na Dodoma, Wachimbaji wadogo wa madini wa mikoa ya Singida na Dodoma, pamoja na wamiliki wa migodi, wasimamizi, Wakaguzi Migodi na Baruti.
Amesema kuwa takwimu za matukio mbalimbali ya ajali yaliyopelekea vifo na majeruhi kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya ajali zote zimesababishwa na kuanguka kwa mashimo ya uchimbaji na kupelekea kukosekana kwa hewa ndani ya mashimo ya uchimbaji, matumizi mabaya ya baruti, utelezi shimoni pamoja na hitilafu za umeme.
"mna wajibu mkubwa wa kuimarisha mfumo wenu wa utendaji kazi kwa kuangalia usalama katika maeneo mnayochimba ili kuhakiksha kuwa taifa halipotezi nguvu kazi ili tuwe na uchimbaji endelevu wa kuimarisha maisha yetu na jamii inayotuzunguka.
Ameendelea kusema kuwa, Mafunzo haya yawe chachu katika utendaji kazi ili yapunguze ajali katika maeneo mnayofanyia kazi, Sisi kama Tume ya Madini tunaamini kuwa uhai wa mchimbaji mmoja una umuhimu mkubwa kuliko uzalishaji wa madini hata wa zaidi ya miaka 10," alisema Prof. Kikula.
Amesema Wachimbaji wengi wamekuwa wakichimba na wanapokoswa madini katika maeneo hayo huacha mashimo na kuhamia sehemu nyingine hali inayopelekea uharibu wa mazingira.
"Naelekeza maafisa madini wote nchini na wamiliki wa leseni wahakikishe kuwa hakuna mashimo yanayoachwa wazi bila kufukiwa ili kuhakikisha usalama na mazingira katika eneo hilo unaachwa katika hali nzuri," alisema Prof. Kikula.
Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba amewaomba Wachimbaji nchini kuendelea kusimamia vizuri maeneo ya kazi pamoja na kuzingatia Usalama, Afya,Usimamizi wa Mazingira na matumizi salama ya baruti migodini.