THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
MINING COMMISSION

TUME YA MADINI YAPONGEZWA UKUSANYAJI WA MADUHULI KWA MWAKA WA FEDHA 2020- 2021


news title here
14
Jul
2021

Yavuka lengo kwa asilimia 111

Kamisheni ya Tume ya Madini, imeipongeza Tume ya Madini kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli ambapo katika mwaka wa fedha 2020-2021 ilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 584.78 sawa na asilimia 111 ya lengo la kipindi husika.

Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 13 Julai, 2021 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula kupitia kikao kazi cha kamisheni ya Tume ya Madini ambacho lengo lake lilikuwa ni kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Madini kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2020- 2021

"Nichukue fursa hii kuupongeza uongozi wa Tume ya Madini chini ya Mhandisi Yahya Samamba, watendaji na watumishi wote wa Tume ya Madini kwa bidii ya kazi na kupelekea lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa kipindi husika kuvukwa, hongereni sanaa," amesema Profesa Kikula.

Katika hatua nyingine Profesa Kikula amesisitiza kuwepo kwa ubunifu kwenye ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2021- 2022 ambapo Tume ya Madini imepangiwa kukusanya shilingi bilioni 650.

Kikao hicho kimeshirikisha makamishna ambao ni pamoja na Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo na mwakilishi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Onarius Njole na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Marko Baruti.

Makamishna wengine ni pamoja na Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), Haroun Kinega na Bi. Janet Reuben Lekashingo.

Watendaji kutoka Tume ya Madini wakiongozwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba walikuwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Huduma za Tume William Mtinya, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Dkt. Abdulrahman Mwanga, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Venance Kasiki pamoja na mameneja na watendaji wengine.