MCHANGO WA SEKTA YA MADINI KWENYE PATO LA TAIFA WAENDELEA KUKUA

Apr
2023
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo amesema kuwa kutokana na usimamizi mzuri unaofanywa na Serikali kwenye Sekta ya Madini kupitia Wizara ya Madini na Tume ya Madini, mabadiliko makubwa yameendelea kuonekana hivyo kupelekea mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa kuendelea kukua huku wawekezaji wengi kutoka nje ya nchi wakiendelea kumiminika kwenye shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini.
Mhandisi Lwamo aliyasema hayo Aprili 25, 2023 kwenye ufunguzi wa kikao cha siku moja cha Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Madini jijini Arusha chenye lengo la kupokea taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Tume, kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Madini pamoja na kuzitatua.
Akielezea mafanikio hayo, alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa ulifikia asilimia 7.2 sambamba na mauzo ya madini nje ya nchi yakiwa ni Dola za Marekani milioni 3,395.3 mwaka 2022 ikiwa ni sawa na asilimia 56 ya mauzo yote ya bidhaa nje ya nchi.
Alifafanua kuwa mafanikio hayo yamepatikana kutokana na kuimarika kwa biashara ya madini nchini kupitia uanzishwaji wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini, kuongezeka kwa kasi ya utoaji wa leseni za madini, kuongezeka kwa udhibiti wa utoroshaji wa madini pamoja na usimamizi bora wa afya na mazingira kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.
“Mwelekeo wa Sekta ya Madini ni kuhakikisha mchango wake kwenye Pato la Taifa unafikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025; haya yanawezekana kutokana na ubunifu na uzalendo mkubwa ambao watumishi wa Tume wamekuwa nao,” alisisitiza Mhandisi Lwamo.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Lwamo alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ina matarajio makubwa sana na Sekta ya Madini kutokana na mchango wake katika makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi, kuchangia fedha za kigeni pamoja na kufungamanisha Sekta ya Madini na sekta nyingine za kiuchumi kwa ujumla.