KASSIM MAJALIWA: KONGAMANO LA MADINI LIMEONGEZA FURSA SEKTA YA MADINI

May
2023
Wachimbaji wadogo wa madini wameshauriwa kulitumia Kongamano la wachimbaji wadogo wa Madini kama fursa ya kujiongezea tija na kujipatia kipato cha mtu mmoja mmoja kupitia mafunzo waliyopata.
Hayo yamebainishwa na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa kwenye kilele cha Wiki ya Maonesho ya Madini wakati akifungua Kongamano la Wachimbaji Wadogo wa Madini na Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) uliofanyika katika ukumbi wa Rock City Mall Jijini Mwanza.
Aidha, Majaliwa amesema kuwa Sekta ya Madini ni Sekta tegemewa inayotarajiwa kuleta matokeo chanya katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kwa Mtanzaniaq mmoja mmoja, Serikali itaendelea kutekeleza adhima yake ya kusimamia na kuwaendeleza wachimbaji wadogo nchini.
"Serikali yetu inathamini sana uchimbaji mdogo kwa kuwa wachimbaji wadogo wanachangia moja kwa moja katika uchumi wetu hivyo Kongamano hili ni muhimu kwa muktadha wa maendeleo ya Sekta ambapo itawaleta karibu wadau wote wa madini na kupata fursa ya kujadiliana ili kupata majibu ya changamoto mbalimbali.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameipongeza FEMATA kwa maandalizi ya Kongamano hilo ambapo amesema mchango wa Sekta ya Madini tangu mwaka 2015 umekuwa ukiimarika mwaka hadi mwaka kutokana na usimamizi thabiti unaotokana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wanayoyatoa kwenye sekta hiyo.
Pamoja na mambo mengine Dkt. Kiruswa amesema lengo la Wizara la kuchangia asilimia 10 kwenye Pato la Taifa ifikapo 2025 litafikiwa na ikiwezekana litachangia zaidi Wizara kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linaendelea kuwaunganisha wachimbaji wadogo na Taasisi za fedha.