THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
MINING COMMISSION

ALIYOZUNGUMZA MHE. JOB NDUGAI SPIKA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE HAFLA YA UTOAJI WA LESENI YA UCHIMBAJI MKUBWA NA UZINDUZI WA TAARIFA YA UHAMASISHAJI UWAZI NA UWAJIBIKAJ


news title here
28
Oct
2021

Nimpongeze Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya kufanikisha uwekezaji huu Mkubwa uwezekane nchini.

Tunakwenda kushuhudia uwekezaji mkubwa utakaotuletea fedha nyingi tutakazozihitaji kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Nishukuru kwa uwepo wa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Christina Mdeme aliyeeleza jinsi ambavyo Ilani ya CCM inakwenda kutekelezwa katika sekta hii ya madini na matarajio ya chama kwenye Sekta ya Madini kutokana na ahadi zilizotolewa kwenye Ilani.

Nikumbushe na kusisitiza suala la Sensa , tupokee jambo hili na kulifanya ajenda ya kudumu kwenye mikutano inayohusisha wananchi wengi waliohudhuria ili kupata elimu ya sensa ili sensa ya mwakani iwe na matokeo mzuri tutakayotumia kutengeneza mipango mizuri zaidi.

Awali ilikuwa ngumu sana kupitisha bajeti ya wizara ya Nishati na Madini kutokana na imani ya watanzania na wabunge kuwa ndogo sana kwenye sekta hii. Sera zetu huko mwanzo zilikuwa hazitufikishi popote tuliona tunaliwa tu.

Tunashukuru kwamba sasa tumekuwa na mikataba inayoeleweka, tumetunga sheria zinazoweza kusimamia rasilimali zetu vizuri, tunapeana leseni hadharani tukiwa tunajua nini kinachokwenda kufanyika tukiwa na maoteo ya nini tutakachokwenda kunufaika nacho.

Trilioni 17 ni karibu nusu ya bajeti yetu kwa miaka ya mradi na ndio maana Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini wapo hapa. Hii ni hatua kubwa sana niwashukuru sana wadau wote wa sekta hii.

Nimefurahi kwamba tupo na Mawaziri kila mmoja akatekeleze na kusimamia eneo lake. Waziri wa Madini uliangalie eneo lingine la madini yanayopatikana Ngara tujue tutanufaikaje.

Tembo Nickel wana kampuni tanzu inayoitwa Tembo Nickel Refining Corporation inayokwenda kuweka mtambo wa kuchenjua madini katika Wilaya ya kahama itakayotusaidia sana kuondoa uwezekano wa kusafirisha makinikia kupeleke nje ya nchi.

Uwekezaji huu unahitaji kila kitu kiende vizuri kuwe na maji na umeme wa uhakika ili manufaa yaonekane.

Kampuni ya Tembo Nickel Corporation Ltd na watumishi watakaoajiriwa na kampuni hii kawajibikeni, msituangushe, mnakwenda kuwakilisha mamilioni ya watanzania hakikisheni mnafanya kazi yenu kwa weledi mkubwa kuhakikisha kila tunachopaswa kukipata kama nchi tunakipata.

Kamati yetu ya Bunge ya Nishati na Madini itakuwa macho sana na mradi huu na ufuatiliaji wake, Mhe. Mwenyekiti huo ni ushauri wangu, tuwe na ufuatiliaji wa karibu, Bunge litawawezesha kila mtakapohitaji kufika na kujionea maendeleo ya mradi huu mnaona shughuli zinavyoendelea na kupokea taarifa.

Wawekezaji niwahakikishie watanzania ni watu wema sana, watu wakarimu sana tafadhali nanyi mwende mkasimame kama mlivyoahidi kufuatana na leseni mnayokabidhiwa leo.

Muanze shughuli mara moja na niwahakikishie kupata kila ushirikiano kupitia Wizara ya Madini.

Ndugu zangu wa Ngara pokeeni wageni hawa kwa mikono miwili mziwahi hizi fursa ili mnufaike na uwekezaji huu mkubwa kihalali.

Halmashauri ya Wilaya ya Ngara mwende mkajipange vizuri kuhakikisha mradi huu unawanufaisha ipasavyo.

TEITI mnatembea na dhana ya Uwajibikaji na Uwazi kwenye sekta hii ya madini, Muendelee kujipanga vizuri katika kufanikisha shughuli hii.

Mnatusaidia sana kujua kama stahiki za serikali zinapokelewa kama inavyostahili.

Natoa wito mkaangalie sababu za tofauti kwenye mapato hayo ili siku moja tufanikiwe kupata kwa asilimia mia moja (100%).

Niwashukuru sana Chuo cha Mzumbe kwa taarifa hii na niwatake muendelee kujiimarisha na kuendelea kutushauri ili tujue namna tutakavyojiimarisha katika kukusanya mapato.