*_Aishukuru GST kwa kufanya utafiti wa madini na kuandaa Ramani ya Jiolojia Zanzibar_*
*_Awakaribisha Wawekezaji Kuwekeza Katika Sekta ya Madini Zanzibar_*
*_Waziri Mavunde asema Wizara itaandaa eneo maalum la kudumu la kufanyia Mikutano ya Madini_*
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mgeni Hassan Juma, amesema kuwa kama ili kufikia azma ya kuwa kitovu cha madini barani Afrika ni lazima kujenga viwanda vitakavyoongeza thamani ya malighafi na kuzalisha bidhaa za mwisho tayari kwa soko la ndani na nje ikiwemo masoko makubwa duniani.
Amesema hayo, leo Novemba 21, 2024, wakati akifunga Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini 2024 uliofanyika kwa siku tatu (Novemba 19-21, 2024) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam,
Mhe. Mgeni ameeleza kuwa mijadala iliyofanyika kupitia Mkutano huo imejikita katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili Sekta ya Madini, hususan katika nyanja za mitaji na teknolojia ya kisasa katika uongezaji thamani madini na kwamba kupitia maazimio yaliyotolewa na washiriki, Serikali imepata mapendekezo yatakayofanyiwa kazi kwa manufaa ya sekta na taifa kwa ujumla.
“Uongezaji thamani madini ni jambo la msingi kwa maendeleo yetu. Tunapaswa kujenga viwanda vitakavyoongeza thamani ya malighafi na kuzalisha bidhaa za mwisho tayari kwa soko la ndani na nje,” amesema Mhe. Mgeni.
Aidha, amesisitiza kuwa, Mkutano huo, uliobebwa na Kaulimbiu ya “Uongezaji Thamani Madini kwa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii”, umekuwa jukwaa muhimu kwa kubadilishana uzoefu, kukuza mitandao na wadau, na kuibua majadiliano ya kitaalamu kuhusu mustakabali wa sekta ya madini nchini hususan katika eneo la uongezaji thamani madini.
Mhe. Mgeni ameongeza kuwa, Kampuni mbalimbali zinazoshughulika na mnyororo wa thamani wa madini zimepata nafasi ya kushiriki mkutano huo, na kwamba matumaini yake ni kuwa zimejifunza kwa kina kuhusu Sera za Madini za Tanzania hivyo zitaendelea kuchangamkia fursa zilizopo ndani ya sekta ya madini hapa nchini.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mgeni ameipongeza na kuishukuru Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa juhudi zake za kufanya utafiti wa madini visiwani Zanzibar na kisha kuandaa ramani ya jiolojia ya visiwa hivyo.
Mhe. Mgeni amesema kuwa kupitia Ripoti ya Utafiti wa Madini Visiwani Zanzibar iliyokabidhiwa na GST hivi karibuni visiwani humo, imesaidia kujua utajiri mkubwa wa rasilimali madini uliopo visiwani humo na kwamba Zanzibar iko tayari kuendeleza rasilimali madini yaliyoanishwa kwa mujibu wa Sheria.
“Kipekee tunaishukuru sana GST kwa hatua kubwa ya kutufanyia utafiti wa Visiwa vyetu. Nitumie fursa hii kuwakaribisha wawekezaji wote waliowekeza katika Sekta ya Madini hapa bara kufikiria kuwekeza pia Zanzibar kwa lengo la kuyaendeleza madini yetu.” Amesema Mhe. Mgeni.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amesisitiza kuwa, Mkutano huo umekuwa na mafanikio makubwa, kwani kwa mwaka 2024 umeleta washiriki zaidi ya 1500 kutoka Afrika na nje ya Africa kwa nia ya kubadilishana uzoefu.
“Kutokana na mahudhurio makubwa ya washiriki, tunafikiria kuwa na eneo letu maalum kwa ajili ya Mikutano ya Sekta ya Madini kama ilivyo kwa Mining Indaba kule Afrika Kusini, na ninawaomba Wakuu wa Mikoa kutenga maeneo maalum katika mikoa yao kwa ajili ya mikutano hii ya madini” amesema Mavunde.
Akizungumzia Kuhusu Sekta ya Madini visiwani Zanzibar, Mhe. Mavunde amesema “Watu wakisikia Zanzibar wanachofikiria ni utalii, lakini miezi michache iliyopita Ripoti ya Utafiti wa Madini kule Zanzibar, Pemba yamegundulika madini tembo (Heavy Mineral Sands) hivyo kupitia rasilimali hiyo tunaamini uwekezaji mkubwa utafika pemba na tutaona manufaa ya uwepo wa rasilimali hizo na itasaidia kufungua uchumi wa Zanzibar“
Naye, Waziri wa Maji, Nishati na Madini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Shaib Hassan Kaduara amesema kuwa, kama taifa moja ni muhimu kuimarisha ushirikiano katika eneo la utafiti wa kina wa madini kwa manufaa ya pande zote na kuongeza kuwa “Ni fahari kubwa kujua tuna rasilimali hizi na tunaahidi kuzisimamia kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo”
Awali akizungumza Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa, Kaulimbiu ya Mkutano “Uongezaji Madini Thamani kwa Maendeleo ya Kiuchumi kwa Jamii” (Mineral Value Addition for Social – Economic Development) ikiwa na lengo la kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini nchini kwa maendeleo ya Kiuchumi kwa Jamii.
Aidha, Dkt. Kiruswa amebaisha kuwa, Kaulimbiu hiyo inaenda sambamba na utekelezaji wa Sera ya Madini ya 2009 ambayo inaitaka Serikali kuhakikisha madini yanayozalishwa nchini yanaongezewa thamani kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi ili kupanua wigo wa mnyororo wa thamani kupitia fursa za ajira na uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata madini nchini.
Mkutano wa mwaka huo wa Uwekezaji wa Katika Sekta ya Madini 2024 umedhihirisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha uwekezaji katika sekta ya madini, na umefungua njia kwa Zanzibar kushiriki kwa kina katika mpango wa maendeleo endelevu ya rasilimali madini.